Jumanne 11 Agosti 2026 - 23:15
Vipengele na hukumu za “Israfu” kwa mtazamo wa Qur’ani na riwaya; kuanzia kupoteza haki hadi kunyimwa uongofu

Leo, katika jamii mbalimbali, utamaduni wa matumizi bora na yenye ufanisi unaenezwa kwa kiwango kikubwa, na matumizi ya kupita kiasi katika nyanja mbalimbali yanapigwa vita. Katika dini tukufu ya Uislamu pia, israfu imelaumiwa vikali katika vyanzo na mafundisho ya Waislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, kuzingatia wastani na kufanya mambo kwa kiasi ni jambo la lazima na la dharura katika kila kazi. Mwanadamu anapovuka mipaka ya wastani, huingia katika israfu. Kwa hakika, israfu ni kosa la mtu binafsi na kijamii ambalo huacha madhara mengi katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii kwa watu.

Leo, katika jamii mbalimbali, utamaduni wa matumizi bora na yenye ufanisi unaenezwa kwa kiwango kikubwa, na matumizi ya kupita kiasi katika nyanja mbalimbali yanapigwa vita, katika dini tukufu ya Uislamu pia israfu imekemewa vikali katika vyanzo na mafundisho ya Waislamu.

Katika Qur’ani na Hadithi, vipengele mbalimbali vya israfu vimeelezwa, na kwa kubainisha uharamu wa jambo hili pamoja na madhara yake, Uislamu unalenga kujenga mazingira ya wastani na kufanya mambo kwa kiasi miongoni mwa watu na katika jamii ya Kiislamu. Kuhusiana na suala hili, tulifanya mazungumzo na Hujjatul-Islam Sayyid Ali Musawi, mmoja wa walimu wa Hawzah ya Qum.

Israfu ni nini na ina maana gani?

Neno hili limetokana na mzizi wa maneno “س ر ف”, na maana yake ni kuvuka mipaka na kupita kiwango katika jambo lolote analolifanya mwanadamu.
Kitabu Mufradat, juzuu ya 2, ukurasa wa 211.

Israfu, mbali na kutumika kumaanisha matumizi mabaya, pia hutumiwa katika mambo yenye upande chanya kama vile kutoa sadaka na kufanya matumizi kwa ajili ya wengine, kama ilivyotajwa katika Suratul-Furqan, aya ya 67:

«وَ الَّذِینَ إِذا أَنْفَقُوا لَمْ یُسْرِفُوا وَ لَمْ یَقْتُرُوا»

“Na wale ambao wanapotumia katika njia ya Mwenyezi Mungu, hawafanyi israfu wala hawafanyi ubahili.”

Lakini katika maana yake ya istilahi, neno israfu hutumiwa hasa katika mambo ya matumizi mabaya na kuvuka kiwango katika jambo lolote.

Tofauti kati ya Israfu na Tabdhiri

Tabdhiri ina maana ya kutawanya na kusambaza kitu, na hutumika kumhusu mtu anayepoteza mali yake bure.
Kitabu Mufradat, juzuu ya 1, ukurasa wa 251.

Tabdhiri katika lugha ya kawaida ni sawa na “kutapanya mali”, ambayo kwa upande wa maana iko karibu na israfu.

Katika israfu, kuzidisha kiwango kunahusu mambo yote, ikiwa ni pamoja na kula, kuvaa, mali na mengineyo, lakini katika tabdhiri, kinachokusudiwa ni kupoteza mali na utajiri tu.

Pamoja na hayo, katika baadhi ya riwaya, maneno israfu na tabdhiri wakati mwingine yametumiwa kwa maana moja. Imam Ali (as) amesema:

«أَلَا وَ إِنَّ إِعْطَاءَ الْمَالِ فِی غَیْرِ حَقِّهِ تَبْذِیرٌ وَ إِسْرَافٌ وَ هُوَ یَرْفَعُ صَاحِبَهُ فِی الدُّنْیَا وَ یَضَعُهُ فِی الْآخِرَهِ»

“Fahamuni kwamba kutoa mali mahali pasipostahili ni ubadhirifu na israfu; jambo hilo humuinua mwenye kufanya hivyo duniani, lakini humshusha daraja Akhera.”
Kitabu Nahjul-Balagha, khutba ya 126.

Hukumu ya Israfu

Dhambi hii, katika maana yake ya istilahi, ni haramu, kwa sababu husababisha kupotezwa kwa haki za Mwenyezi Mungu na haki za watu. Ni kupoteza haki ya Mwenyezi Mungu kwa sababu mtu anapoteza neema za Mwenyezi Mungu; na ni kupoteza haki ya watu kwa sababu huenda mtu mwingine akawa mhitaji, huku mwenye kufanya israfu akitumia kupita kiasi kitu alichonacho na kukipoteza.

Suala la Israfu katika Qur’ani Tukufu

Katika Qur’ani Tukufu, neno hili na maneno yanayotokana na mzizi wake yametajwa mara 23, likitumika kwa maana ya jumla na pia kwa maana yake ya istilahi.

«وَ لا تُطِیعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِین‌»

“Wala msitii amri ya watu wafanyao israfu.”
Suratush-Shu‘ara, aya ya 151.

«وَ کُلُوا وَ اشْرَبُوا وَ لا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لا یُحِبُّ الْمُسْرِفِین‌»

“Na kuleni na kunyweni, wala msifanye israfu. Hakika Yeye hawapendi wafanyao israfu.”
Suratul-A‘raf, aya ya 31.

«إِنَّ اللَّهَ لا یَهْدِی مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ کَذَّاب‌»

“Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi mwenye kufanya israfu na mwongo.”
Surah Ghafir, aya ya 28.

Israfu katika riwaya za Ahlul-Bayt (as)

Katika vyanzo vya riwaya pia, kuna hadithi nyingi zinazohusu suala la israfu na ubadhirifu.

Imam Sadiq (as) amesema katika hadithi:

«ادنی الاسراف هراقه فضل الاناء و ابتذال ثوب الصون و القاء النوی»

“Kiwango cha chini kabisa cha israfu ni kumwaga maji yanayobaki katika chombo baada ya kunywa; kutumia vazi la kazi na vazi la kutoka nje kuwa vazi moja; na kutupa kokwa ya tende baada ya kula tende.”
Kitabu Wasa’il al-Shi‘a, Hadithi ya 3, mlango wa 28, ukurasa wa 374.

Katika hadithi hii, Imam amebainisha mipaka ya israfu kwa kutoa mifano, na jambo hili linaweza kuenezwa na kutumika katika masuala mengine.

Imam Ali (as) anataja alama za mtu anayefanya israfu kama ifuatavyo:

«لِلْمُسْرِفِ ثَلَاثُ عَلَامَاتٍ یَأْکُلُ مَا لَیْسَ لَهُ وَ یَلْبَسُ مَا لَیْسَ لَهُ وَ یَشْتَرِی مَا لَیْسَ لَه‌»

“Mwenye kufanya israfu ana alama tatu: anakula kisicho chake, anavaa kisicho chake, na hununua kisicho chake.”
Kitabu Bihar al-Anwar, juzuu ya 72, ukurasa wa 304.

Bila shaka, maana ya “kisicho chake” hapa ni kwamba jambo hilo halilingani na hadhi yake na ni zaidi ya kiwango chake.

Katika hadithi nyingine, Imam Ali (as) anaeleza kuwa; kufanya mambo kwa kiasi huleta utajiri, huku israfu ikiangamiza utajiri.
Kitabu Bihar al-Anwar, juzuu ya 68, ukurasa wa 347.

Aina za Israfu

Israfu, ambayo maana yake ni kutoka katika mipaka ya wastani, ina mifano mingi, miongoni mwao ikiwa ni:

1. Israfu ya kiitikadi

Katika aya za Qur’ani Tukufu, hata kufanya dhambi kumetajwa kuwa ni israfu, kwa sababu mwanadamu amevuka kiwango cha wastani.

«وَ کَذلِکَ نَجْزِی مَنْ أَسْرَفَ، وَ لَمْ یُؤْمِنْ بِآیاتِ رَبِّهِ، وَ لَعَذابُ الْآخِرَهِ أَشَدُّ وَ أَبْقی‌»

“Na hivyo ndivyo tunavyomlipa aliyefanya israfu na asiamini ishara za Mola wake; na bila shaka adhabu ya Akhera ni kali zaidi na yenye kudumu zaidi.”
Surah Taha, aya ya 127.

2. Israfu ya kimaadili na kitabia

Mtu anapojitenga na mipaka ya kimaadili ya mwanadamu, israfu hutokea, upotovu wa kijinsia, tabia mbaya na kila aina ya maadili yasiyofaa huingia katika israfu.

Katika Qur’ani Tukufu, kuhusiana na watu wa Lut, Mwenyezi Mungu aliwaita kuwa ni watu wafanyao israfu kwa sababu walivuka mipaka ya Sheria na akili kwa vitendo vyao viovu.

«إِنَّکُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجالَ شَهْوَهً مِنْ دُونِ النِّساءِ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ مُسْرِفُون‌»

“Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake; bali nyinyi ni watu wafanyao israfu.”
Suratul-A‘raf, aya ya 82.

3. Israfu ya kiuchumi

Israfu katika mambo mengi yanayotokea katika maisha ya kila siku inaingia katika kundi hili, kama vile:

- Kuharibu vitu ambavyo bado vinaweza kutumika.
- Kutimiza au kununua mahitaji ambayo hayahitajiki.

Imam Sadiq (as) amesema: “Kwa mwanamume ni lazima awe na godoro moja, godoro kwa ajili ya familia yake, na godoro kwa ajili ya mgeni wake; godoro la ziada ni la Shetani.”
Kitabu Bihar al-Anwar, juzuu ya 76, ukurasa wa 321.

Kutumia kitu ambacho kina madhara kwa mwili, iwe ni kwa kiwango kidogo au kikubwa, pia ni miongoni mwa mifano ya jambo hili. Kwa mfano, matumizi ya pombe, ambayo hata kiwango kidogo chake kina madhara kwa mwili, ni miongoni mwa mifano hiyo.

Kutumia kitu kupita kiasi katika kila jambo, kama vile kula, kunywa na mavazi.

Kununua vitu vinavyopita hadhi ya mwanadamu, kama vile nyumba kubwa kupita kiasi, chombo cha usafiri na mambo mengine.

Mizizi ya Israfu

Miongoni mwa mizizi ya jambo hili ni kama mambo yafuatayo:

Mizizi ya kiitikadi

Miongoni mwa mizizi ya kiitikadi iliyotajwa katika Qur’ani Tukufu na riwaya za Ahlul-Bayt (as) ni mambo yafuatayo:

Ujinga

Miongoni mwa mambo yanayomsababisha mwanadamu kufanya makosa katika kila nyanja ni ujinga na kutokuwa na elimu.

Mtu anapokuwa mjinga kuhusu namna ya kupata mali halali, huangukia katika israfu, wakati utajiri unapomfikia mtu kwa njia ya urithi, na hajafanya juhudi yoyote kuupata utajiri huo, bila shaka hatauthamini na hatimaye jambo hilo linaweza kumpeleka kwenye israfu.

Kufuatilia matamanio

Katika aya ya 81 ya Suratul-A‘raf, kutawaliwa na matamanio kumetajwa kuwa sababu ya watu wa Lut kuelekea katika israfu:

«إِنَّکُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِنْ دُونِ النِّسَاءِ ۚ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ مُسْرِفُونَ»

“Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake; naam, nyinyi ni watu wafanyao israfu.”

Kughafilika na kumkumbuka Mwenyezi Mungu

Katika aya isemayo:

«لا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنا قَلْبَهُ عَنْ ذِکْرِنا وَ اتَّبَعَ هَواهُ وَ کانَ أَمْرُهُ فُرُطا»

“Wala usimtii yule ambaye tumeufanya moyo wake kuwa ghafilifu na ukumbusho Wetu, akafuata matamanio yake, na jambo lake likawa limepita mipaka.”

Wale ambao wameghafilika na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na wakafuata matamanio yao huangukia katika hali ya kupita mipaka.
Suratul-Kahf, aya ya 28.

Mizizi ya kisaikolojia

Kiburi

Watu wanaokumbwa na hali ya kiburi na kujiona kuwa ni bora kuliko wengine daima hujitahidi kuonesha ubora wao kwa wengine kwa njia yoyote ile, katika hali hii mtu huvuka mipaka na kusababisha israfu.

Kujionyesha

Wakati mwingine mtu anapotaka kujithibitisha na kuficha kushindwa na hali za udhalili alizowahi kupitia, jambo hilo pia humpeleka katika matumizi ya kupita kiasi.

Wasiwasi wa kupita kiasi

Miongoni mwa mambo yanayohusika sana katika suala hili ni tatizo la wasiwasi wa kupita kiasi. Mtu anapokuwa na hali hii, hutumia fedha kupita kiasi au huandaa maandalizi mengi sana katika hafla na mapokezi, na kutokana na hali yake ya wasiwasi wa kupita kiasi, hata vitu vilivyobaki huvipoteza.

Mizizi ya kijamii na kiutamaduni

Malezi ya kifamilia

Mwanadamu anapokuwa hajajifunza kufanya mambo kwa kiasi katika mazingira ya familia, na badala yake akaona tabia ya kufanya israfu, naye katika maisha yake huangukia katika israfu, na jambo hili huwa la kawaida kwake.

Kuiga

Katika jamii, wakati ambapo mifano ya kijamii pamoja na viongozi na watawala wa serikali wanakuwa wameathiriwa na utamaduni wa matumizi ya kupita kiasi, bila shaka watu wa jamii hiyo pia, kwa kuwaiga, huangukia katika israfu.

Kama Qur’ani Tukufu inavyosema:

«وَ لا تُطِیعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِین‌»

“Wala msitii amri ya wafanyao israfu.”
Suratush-Shu‘ara, aya ya 151.

Umaskini wa kiutamaduni na ukosefu wa uelewa katika jamii

Wakati katika jamii fulani mafunzo sahihi kuhusu namna bora ya matumizi hayajaelezwa, jamii hiyo huenda kuelekea katika utamaduni wa matumizi ya kupita kiasi. Suala hili, linalotokana na umaskini wa kiutamaduni, husababisha kuangamia kwa jamii hiyo.

Madhara ya Israfu

Katika matumizi mabaya na utamaduni wa kufanya israfu, mwanadamu hupata hasara nyingi katika mambo ya kimwili na kiroho, miongoni mwao zikiwa ni:

Madhara ya kimwili

Umaskini na ufukara

Kutokana na tamaa kutaka zaidi na matumizi yasiyo na mipaka, hatimaye mwanadamu hufikia hali ya ufukara. Kukosekana kwa mpango wa kiuchumi katika maisha pamoja na tamaa hizi na matumizi ya kupita kiasi huleta matatizo mengi, yakiwemo umaskini.

Israfu husababisha kukosekana kwa baraka katika maisha

Jambo hili husababisha kupotezwa kwa haki za wengine. Israfu husababisha kupotea kwa rasilimali za kitaifa za jamii, jambo ambalo huleta hasara zisizoweza kurekebishwa kwa jamii hiyo.

Aidha, husababisha mashindano ya kuoneshana uwezo na utajiri, pamoja na matukio mengi yasiyofaa katika jamii.

Madhara ya kiroho

Kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu Mkarimu hawapendi wafanyao israfu.

«وَ هُوَ الَّذِی أَنْشَأَ جَنَّاتٍ مَعْرُوشَاتٍ وَ غَیْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَ النَّخْلَ وَ الزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُکُلُهُ وَ الزَّیْتُونَ وَ الرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَ غَیْرَ مُتَشَابِهٍ ۚ کُلُوا مِنْ ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُوا حَقَّهُ یَوْمَ حَصَادِهِ ۖ وَ لَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا یُحِبُّ الْمُسْرِفِینَ»

“Na Yeye ndiye aliyeumba bustani zenye miti iliyoinuliwa kwenye nguzo na zisizo kwenye nguzo, na mitende, na mimea yenye mazao ya aina mbalimbali, na mizaituni na mikomamanga yenye kufanana na isiyofanana. Kuleni katika matunda yake yanapozaa, na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake; wala msifanye israfu. Hakika Yeye hawapendi wafanyao israfu.”
Suratul-An‘am, aya ya 141.

Israfu humfanya mwanadamu kunyimwa uongofu wa Mwenyezi Mungu

«وَ قَالَ رَجُلٌ مُؤْمِنٌ مِنْ آلِ فِرْعَوْنَ یَکْتُمُ إِیمَانَهُ أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَنْ یَقُولَ رَبِّیَ اللَّهُ وَ قَدْ جَاءَکُمْ بِالْبَیِّنَاتِ مِنْ رَبِّکُمْ وَ إِنْ یَکُ کَاذِبًا فَعَلَیْهِ کَذِبُهُ وَ إِنْ یَکُ صَادِقًا یُصِبْکُمْ بَعْضُ الَّذِی یَعِدُکُمْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا یَهْدِی مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ کَذَّابٌ»

“Na mtu mmoja muumini miongoni mwa watu wa Firauni, aliyekuwa akificha imani yake, alisema: Je, mtamuua mtu kwa sababu tu anasema: ‘Mola wangu ni Mwenyezi Mungu,’ hali amekuleteeni hoja zilizo wazi kutoka kwa Mola wenu kwa ajili ya kuwaongozeni? Ikiwa yeye ni mwongo, basi uongo wake utakuwa juu yake mwenyewe; lakini ikiwa ni mkweli, baadhi ya yale anayokuahidini yatakupateni, na nyinyi nyote mtaangamia. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi kamwe mtu mwenye kufanya israfu na mwongo.”
Surah Ghafir, aya ya 28.

Dua ya mtu anayefanya israfu haikubaliwi

«لَا یُسْتَجَابُ لَهُمْ أَحَدُهُمْ کَانَ لَهُ مَالٌ فَأَفْسَدَهُ»

“Dua yao haijibiwi; miongoni mwao ni yule aliyekuwa na mali kisha akaipoteza na kuiharibu.”
Kitabu Usul al-Kafi, juzuu ya 4, ukurasa wa 56.

Mwenye kufanya israfu ni miongoni mwa watu wa Motoni

«وَ أَنَّ الْمُسْرِفِینَ هُمْ أَصْحابُ النَّار»

“Na hakika wafanyao israfu ndio watu wa Motoni.”
Surah Ghafir, aya ya 43.

Adhabu kali zilizoahidiwa kwa wafanyao israfu

«مُسَوَّمَهً عِنْدَ رَبِّکَ لِلْمُسْرِفِین‌»

“Zikiwa zimetiwa alama na Mola wako kwa ajili ya wafanyao israfu.”
Surah Adh-Dhariyat, aya ya 34.

«وَ کَذلِکَ نَجْزِی مَنْ أَسْرَفَ وَ لَمْ یُؤْمِنْ بِآیاتِ رَبه وَ لَعَذابُ الْآخِرَهِ أَشَدُّ وَ أَبْقی‌»

“Na hivyo ndivyo tunavyomlipa aliyefanya israfu na asiamini ishara za Mola wake; na bila shaka adhabu ya Akhera ni kali zaidi na yenye kudumu zaidi.”
Surah Taha, aya ya 127.

Njia za kuzuia Israfu

Njia za kuzuia israfu zinaweza kugawanywa katika makundi mawili makuu:

Sababu za ndani

b

Miongoni mwa njia za kukabiliana na madhara ya kimaadili na kiuchumi na kuweka katika jamii maadili ya Kiislamu ni kuimarisha imani juu ya Mwanzo na Marejeo.

Wakati roho na nafsi ya mwanadamu inapokuwa imefungamana na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na maadili ya Kiislamu, mwanadamu hatafuata tena maovu kama vile israfu.

Kurejea katika aya na riwaya

Mwanadamu kwa kurejea katika aya za Qur’ani Tukufu na riwaya za Ahlul-Bayt (as), ambapo imeelezwa kwa wingi kuhusu vipengele mbalimbali vya israfu, dhambi yake na adhabu zake, hujilinda dhidi ya kujichafua kwa dhambi ya israfu.

Kuimarisha maadili ya kidini

Kuimarisha maadili kama vile kujinyima kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (zuhd), kuridhika na alichonacho (qana‘a) na kuwa mwenye kushukuru ni miongoni mwa sababu za ndani za kupambana na israfu.

Sababu za nje
Kuinua kiwango cha uelewa

Kwa upande mwingine, miongoni mwa sababu muhimu zinazosababisha israfu ni ujinga na kutokuwa na elimu. Kwa kuongeza uelewa miongoni mwa watu na kueleza madhara yake makubwa, suala la israfu linaweza kupungua katika jamii.

Kuamrisha mema na kukataza maovu

Miongoni mwa hatua zinazosaidia kuhifadhi alama na mafundisho ya dini na kuondoa madhambi kama vile israfu katika jamii ni kuamrisha mema na kukataza maovu.

Kutoa mfano sahihi wa matumizi na kuanzisha uhamasishaji

Kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu kuzingatia mfumo sahihi wa matumizi na kuhifadhi rasilimali na maadili, kuchukua hatua za kisheria na kiutendaji dhidi ya wafanyao israfu, pamoja na kampeni na matangazo kupitia vyombo vya habari, kunaweza kuwa na ufanisi mkubwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha